Muongozo wa Uratibu wa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Serikali za Mitaa wapata nguvu za wadau

Ofisi ya Rais-Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora (OR-KSUUB) kupitia Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria imeendesha mkutano wa siku moja wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu muongozo wa uratibu wa huduma za msaada wa kisheria katika Serikali za Mitaa.

Lengo kuu la mkutano huo ni kupokea maoni ya wadau kwa ajili ya kuimarisha rasimu ya awali ya muongozo huo unaotokana na utekelezaji wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Msaada wa Kisheria Nam. 13 ya mwaka 2018 kinachomtaka Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kwa kushauriana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kumpa kazi Afisa Sheria wa Serikali za Mitaa kuwa Afisa wa msaada wa kisheria kwa lengo la kuratibu ipasavyo huduma za msaada wa kisheria ndani ya Mamlaka ya mipaka ya Serikali za Mitaa husika.

Akifungua mkutano huo uliofanyika tarehe 07 Septemba 2021 katika Ukumbi wa Wizara –Mazizini, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria ndugu Hanifa Ramadhan Said alisema kuwa muongozo huo utasaidia katika uratibu mzuri wa upatikanaji wa msaada wa kisheria katika Serikali za Mitaa na pia utekelezaji mzuri wa Sheria ya Msaada wa Kisheria.

‘Ni muhimu kutoa maoni ambayo yataweza kuimarisha muongozo huu ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa na kutatua changamoto zilizopo’ alisisitiza.

Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha maafisa Sheria wa Halimashauri, Wenyeviti wa masheha, Watoaji msaada wa Kisheria wakiwemo Wasaidizi wa Sheria, maafisa ustawi wa jamii, Mkuu wa Polisi Dawati Wilaya ya Mjini, Afisa Elimu Mkoa, Jumuiya ya waandishi wa habari na watumishi wa OR-KSUUB.

Washiriki walipata nafasi ya kuelewa muongozo huo kwa kina baada ya kupatiwa uwasilishaji mdogo unaohusu muongozo huo uliotolewa na Afisa Sheria wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria ndugu Salma Suleiman Abdulla.

Nao, washiriki hao walitoa maoni yao juu ya kuimarisha rasimu ya muongozo huo pamoja na kutoa mapendeezo kwa Idara juu ya upatikanaji wa elimu juu ya muongozo huo pale utakapokamilika kwa watendaji mbali mbali wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa na wananchi kwa ujumla ili uweze kufahamika na kutekelezeka.

Vile vile, walishauri suala la kufanyiwa tathmini na mapitio muongozo huo pale utakapokamilika na kujumuisha waratibu wa wanawake na watoto kwenye muundo wa Kamati ya Shehia.

Mkutano huu ni moja katika utekelezaji wa shughuli za mpango kazi wa Idara ya Katiba na Msada wa Kisheria kwa mwaka 2020/2021.

Close
Close