Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefanya bidii kubwa kuhakikisha misingi ya utawala bora inafuatwa ili kukuza uchumi na kujenga jamii yenye imani, upendo na mshikamano baina yao, serikali na nchi yao kwa jumla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakili, Kikwajuni mjini Zanzibar katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu.

Katika hotuba hiyo, Rais Dk. Shein aliitaja misingi hiyo kuwa ni ushirikishwaji wa umma, utawala wa sheria, haki na usawa kwa watu wote,uwazi katika kuendesha shughuli za maendeleo pamoja na uwajibikaji katika utendaji na uadilifu.

Rais Dk. Shein alieleza hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali kuona kwamba utawala bora unaimarika ikiwa ni pamoja na kupitisha Sera ya Utawala bora ya mwaka 2011, ambayo utekelezaji wake unasaidia katika kuyafikia malengo ya mkataba wa haki za binaadamu na ule wa mapambano dhidi ya rushwa.

Alieleza kuwa Tanzania ni nchi ya mwanzo kuanzisha Wizara ya Utawala Bora katika nchi za Bara la Afrika hatua ambayo imeijengea sifa kubwa ndani na nje ya Afrika.

Close
Close