HAROUN /SAUDI ARABIA

news phpto

Picha kwa hisani ya Kitengo cha Habari

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mwalimu Haroun Ali Suleiman ameeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Saudi arabia ambazo zimekuwa zikichangia kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hiyo na zanzibar .

Waziri Haroun ametoa tamko hilo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa hijja na Umra Wa Saudi Arabia Dk.Abdulfatah Suliman Mashat wakati alipotembelea mji wa makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra.

Katika mazungumzo hayo, ambayo yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Balozi Ali Jabir Mwadini, Mwalim Haroun alisema kwamba Serikali ya Zanzibar inathamini ushirikiano uliopo baina ya pande mbili hizo.

Alibainisha kwamba, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakipongeza na kufarijika juhudi zinazofanywa na Serikali ya Saudi Arabia katika kukamilisha hatua za kufungua Akaunti Maalumu ya Hijja ambayo itatumiwa na Mahujaji wa Zanzibar kwa ajili ya matayarisho ya safari ya Hijja.

Akaunti hiyo itasaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza katika suala zima la malipo na ushughulikiaji wa miamala mengine muhimu ya kifedha kwa Mahujaji wa Zanzibar.

Wazir Haroun amezipongeza taasisi mbali mbali za dini za Nchi hiyo kwa kushirikiana na taasisi za Zanzibar katika usafirishaji na usambazaji wa misaada mbali mbali inayotolewa na Nchi hiyo kwa Wananchi wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na sadaka inayoletwa Zanzibar kila mwaka baada ya kukamilika ibada ya Hijja

Wazir Haroun alisisitiza juu ya umuhimu wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja baina ya Saudi Arabia na Zanzibar kwa lengo la kuimarisha biashara, utalii pamoja na kurahisisha usafiri hasa kwa mahujaji na waumini mbali mbali wanaosafiri kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Ummra.

Waziri wa Hijja na Umra Dk. Abdulfattah Suliman Mashat aliahidi kwamba, nchi hiyo inafanya juhudi mbali mbali katika kuhakisha uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Zanzibar na Saudi Arabia unaimarishwa na kuendelezwa katika sekta mbali mbali, zikiwemo elimu, ujenzi wa miundombinu pamoja na usafirishaji.

Aliahidi kulifuatilia ombi la kuanzishwa usafiri wa moja kwa moja kati ya Saudi Arabia na Zanzibar ili kuimarisha na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya pande zote mbili.

Waziri Haroun alitoa pongezi maalum kwa Maofisa wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kwa juhudi zao katika kuimarisha uhusiano baina ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Umra ni kuizuru nyumba takatifu (alkaaba) inayotekelezwa na waumin wa kiislamu wakati wowote wanapotaka kwa kutekeleza matendo ya ibada maalum

Close
Close