SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA

Siku 100 za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano Tanzania imefanikiwa kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aids Campaign) kwa kuhakikisha huduma hiyo inawafikia karibu Wananchi wa Unguja na Pemba. Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 03 Machi 2026 katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusiana na siku 100 za Mafanikio ya Uongozi wa Dkt. Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema jumla ya wananchi 680,184 wamepata huduma hiyo, wa kiwemo wanaume 312,954 na wanawake 367,230 kwa Unguja na Pemba. Amesema katika kampeni hiyo jumla ya migogoro 749 imepokelewa ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, ajira, udhalilishaji na ukatili wa kijinsia pamoja na matunzo ya watoto ambapo migogoro 259 imetatuliwa papo kwa hapo. Aidha, Waziri Haroun ameeleza kuwa Serikali imeimarisha muhimili wa mahakama kwa kuongeza idadi ya majaji mahakamani na kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi katika mikoa mbalimbali ndani ya Zanzibar hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji rahisi wa haki kwa wananchi. “Juhudi kubwa zimefanywa za kuimarisha muhimili wa mahakama kwa kuongeza idadi ya majaji kutoka majaji 8 mwaka 2021 hadi kufikia majaji 14 mwaka 2025, wakiwemo wanawake 5 na wanaume 9, miundombinu ya mahakama inaendelea kuimarishwa kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za mikoa na wilaya kwa Unguja na Pemba ili kuimarisha upatikanaji wa haki na kusogeza utoaji wa huduma karibu na wananchi" ameeleza Waziri Haoun. Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uendeshaji wa kesi, jumla ya kesi 7,352 zimesikilizwa, huku idadi ya kesi ikipungua kwa asilimia 30.7 katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023. Waziri Haroun pia amezungumzia Afisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Dkt. Haroun kuwa Ofisi hiyo kupitia Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imefanikiwa kuokoa na kudhibiti jumla ya sh. Bilioni 27.82 na dola za kimarekani 35,341 kati ya fedha hizo bilioni 26.37 na dola za kimarekani 30,542 zilirudishwa Serikalini na bilioni 1.45 na dola za kimarekani 4,799 zilirejeshwa kwa wananchi. “Vile vile katika kipindi cha miaka mitano Ofisi kupitia ZAECA ilifanikiwa kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo 233 Unguja na Pemba yenye wastani wa thamani ya sh.trilion 2.29 na dola za Kimarekani milioni 85942 ili kuona utekelezaji wake kwa kuzingatia ubora wake na thamani halisi ya fedha katika miradi hiyo” amefahamaisha Waziri Haroun. Kwa upande wa ZAECA, Wizara imeendelea kufanya kazi kwa karibu na miradi mikubwa ya Serikali kwa kuweka utaratibu wa ufuatiliaji ili kupunguza vitendo vya rushwa na kuhakikisha fedha za Serikali zinalindwa na kutumika ipasavyo. Waziri amesema Serikali ina mpango wa kufanya tathmini ya utendaji wa watumishi ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, ukizingatia maslahi ya wafanyakazi kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma. Hivyo, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali zinazowahusu baadhi ya watumishi na viongozi, na kusisitiza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria. VIlevile, Waziri Haroun amewataka watumishi wa umma kufuata Sheria na Kanuni za kiutumishi na kudumisha uwajibikaji ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu.