SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA

Uzinduzi wa Maabara ya Utafiti wa Afya ya Wanyama

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman, amezindua rasmi Maabara ya Utafiti wa Afya ya Wanyama iliyopo Kizimbani/Dole, Wilaya ya Magharibi “A”, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Dkt. Haroun amesema uanzishwaji wa maabara hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya mifugo na afya ya wanyama, sambamba na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuhakikisha maendeleo endelevu yanawafikia wananchi katika ngazi zote. Amesema uwekezaji katika tafiti za afya ya wanyama una mchango mkubwa katika kulinda uchumi wa wafugaji, kuongeza uzalishaji wa mifugo na kuhakikisha usalama wa chakula kwa jamii. Dkt. Haroun ameeleza kuwa maabara hiyo itawezesha wataalamu kufanya uchunguzi wa kisayansi kwa haraka na kwa usahihi, kufuatilia na kudhibiti magonjwa ya wanyama yanayoathiri mifugo, pamoja na kusaidia upatikanaji wa taarifa na takwimu zitakazosaidia Serikali katika kupanga sera, mikakati na programu mbalimbali za maendeleo ya sekta ya mifugo. Ameongeza kuwa uwepo wa maabara hiyo utapunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali za kusafirisha sampuli za wanyama kwenda maeneo mengine nje ya wilaya au nje ya Zanzibar kwa ajili ya uchunguzi, hali ambayo ilikuwa ikigharimu muda na fedha nyingi kwa wafugaji na taasisi husika. Kupitia maabara hiyo, huduma zitapatikana karibu na wananchi na kwa gharama nafuu. Aidha, Waziri Haroun amewasisitiza wataalamu wa afya ya wanyama, watendaji wa Serikali na wadau wa sekta ya mifugo kuitunza na kuitumia miundombinu hiyo kwa ufanisi, uadilifu na kuzingatia maadili ya taaluma, ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa na kuchangia maendeleo ya kweli kwa jamii. Kwa upande wao, viongozi wa sekta ya mifugo na afya ya wanyama wameeleza kuwa maabara hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wafugaji wa Wilaya ya Magharibi “A” na Zanzibar kwa ujumla, kwani itaongeza uwezo wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko, kuboresha ubora wa mifugo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo na hatimaye kuinua kipato cha wananchi. Uzinduzi wa maabara ya utafiti wa afya ya wanyama umefanyika katika kipindi ambacho Zanzibar inaendelea kuadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu, maadhimisho yanayoendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma za kijamii, kuwekeza katika sayansi na teknolojia, pamoja na kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanawanufaisha wananchi wote.