Waziri Haroun atembelea na kushiriki katika Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar (ZITF)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Dkt. Haroun Ali Suleiman, ametembelea na kushiriki katika Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar (ZITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho Dimani, Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.Maonesho hayo yalianza tarehe 29 Disemba 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Januari 2026, yakiwa ni sehemu muhimu ya maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maonesho hayo yamelenga kukuza biashara, uwekezaji, ubunifu na ushindani wa bidhaa na huduma, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Zanzibar na nchi mbalimbali duniani. Katika ziara yake, Mheshimiwa Waziri alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yanayoshirikisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, kampuni binafsi, wajasiriamali, pamoja na taasisi za Serikali. Akiwa katika mabanda hayo, Mheshimiwa Waziri alipata maelezo juu ya shughuli, bidhaa na huduma zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo, huku akiwapongeza kwa juhudi zao katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa. Mheshimiwa Dkt. Haroun Ali Suleiman alieleza kuwa maonesho ya ZITF ni jukwaa muhimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji kukutana, kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya na kujitangaza katika masoko ya ndani na ya kimataifa. Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira bora ya kisheria, kiutawala na kibiashara ili kuchochea uwekezaji na ukuaji wa sekta binafsi. Aidha, Waziri huyo alibainisha kuwa kupitia maonesho hayo, wananchi hususan vijana na wanawake wanapata fursa ya kujifunza, kujiajiri na kukuza vipaji vyao vya ujasiriamali, jambo linalochangia kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza kipato cha wananchi. Alitoa wito kwa wajasiriamali wa ndani kuendelea kuboresha ubora wa bidhaa na huduma zao ili ziweze kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa. Katika mazungumzo yake na washiriki wa maonesho hayo, Mheshimiwa Waziri alihimiza taasisi za Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria, taratibu na fursa mbalimbali zinazohusiana na biashara, uwekezaji na utawala bora, ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanazingatia misingi ya haki, uwazi na uwajibikaji. Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar yalifunguliwa rasmi tarehe 7 Januari 2026 na yameendelea kuvutia idadi kubwa ya wageni na washiriki kutoka sekta mbalimbali. Maonesho hayo yanathibitisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi shindani, kukuza biashara na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na nje ya Afrika.