SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA

Ufunguzi wa Mafunzo kwa Wakuu wa Taasisi zinazojitegemea

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh.Hemed Suleiman Abdulla, ameziagiza taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinakitumia Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) kwa mafunzo mbalimbali yanayohitajika kwa watumishi wao, ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi. Mhe.Hemed ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya Wakuu wa Taasisi zinazojitegemea za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyofanyika katika ukumbi wa Tume ya Uchaguzi uliopo Maisara, Mjini Zanzibar. Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uwezo wa viongozi hao katika usimamizi, maamuzi ya kimkakati na uendeshaji wa taasisi kwa misingi ya utawala bora. Amesema IPA ni chuo chenye uwezo, uzoefu na rasilimali za kutosha kutoa mafunzo yenye tija kwa watumishi wa umma, akibainisha kuwa kimejenga ushirikiano imara na vyuo na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi,ushirikiano huo umewezesha chuo hicho kuendana na mabadiliko ya kiutendaji na kiteknolojia yanayoendelea duniani. Makamu wa Pili wa Rais amesisitiza kuwa uwekezaji katika mafunzo ni hatua muhimu ya kujenga utumishi wa umma ulio imara, wenye weledi na unaoendana na matarajio ya wananchi. Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea kusisitiza mageuzi katika sekta ya umma kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo na kuimarisha utoaji wa huduma bora. Amesisitiza kuwa uendeshaji bora wa Serikali unaanzia kwa viongozi waliothibitishwa kitaaluma na wenye maadili mema na kuongeza kuwa mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea ubora wa uongozi wake na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa wakati. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dkt. Haroun Ali Suleiman, amesema mafunzo hayo kwa wakuu wa taasisi ni fursa muhimu ya kukumbushana kiutendaji, kuimarisha uwajibikaji na kujenga mshikamano katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), Dkt. Abdul-Hamid Yahya Mzee, amesema chuo hicho kitaendelea kutoa mafunzo hayo kwa ngazi zote zilizobaki za uongozi, kuanzia ngazi za juu hadi za kati, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu misingi ya uongozi na utendaji bora. Ameeleza kuwa IPA imejipanga kuendelea kubuni programu mpya za mafunzo zinazoendana na mahitaji ya sasa ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na usimamizi wa rasilimali watu. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika uendeshaji wa taasisi za umma, kuongeza uwajibikaji, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hatua ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya maendeleo ya Zanzibar.