SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA

MFUMO WA eZPSC WAZINDULIWA KUIMARISHA HUDUMA ZA KAMISHENI YA UTUMISHI WA UMMA ZANZIBAR.

Ni muhimu kutumia Mifumo ya Kieletroniki kwa watumishi wa Serikali katika kurahisisha taarifa na kuondoa usumbufu ili kuwepo ukweli na uwajibikaji na kuweza kuleta maendeleo katika jamii. Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman wakati alipokuwa akizindua Mfumo wa Kielektroniki wa eZPSC unaosimamiwa na Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar. Dkt. Haroun amesema kuwepo kwa Mifumo hiyo ni hatua muhimu katika kuifanya Kamisheni kuwa na utaratibu wa kutumia Teknolojia ya Kidijitali inayoendana na juhudi za Serikali kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi na watumishi wa umma. Kwa upande wake, Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Ndg. Kubingwa Mashaka Simba amesema, mfumo huo utasaidia kurahisisha ufuatiliaji wa rufaa , malalamiko na mapendekezo kwa lengo la kuboresha taarifa zitakazowasilishwa na kushughulikiwa kwa haraka. Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) Dkt. Said Seif Said ameeleza matumizi ya Teknolojia na Mifumo ya Kidijitali ni sehemu muhimu inayopaswa kuendelea kupewa kipaumbele ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na taarifa, pamoja na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali. Nae Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Ndg. Fatma Gharib Bilali ameipongeza Kamisheni kwa kuandaa Mifumo ya Kidijitali inayotarajiwa kusaidia kupunguza utegemezi katika ofisi ya Kamisheni kupitia Idara ya Miongozo na Miundo, Idara ya Rufaa na Malalamiko pamoja na Idara ya Ukaguzi kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma . Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Tume ya Uchaguzi Maisara Zanzibar tarehe 31 Agosti 2026.