UGENI WA BALOZI MDOGO WA JAMUHURI YA WATU WA CHINA ZANZIBAR KONSELI. LI QUINGHUA KATIKA OFISI YA RAIS KATIBA, SHERIA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Serikali ya China ambao ulikuwepo tokea mwaka 1964 uliosaidia katika kukuza maendeleo mbalimbali ndani ya Zanzibar hususan kwenye Sekta za Afya, Elimu, Utawala Bora, Mahakama na Mapambano dhidi ya Rushwa. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman wakati wa mazungumzo yake na Balozi mdogo wa Jamuhuri ya watu wa China Zanzibar Konseli. Li Qianghua, aliyefika ofisini kwake tarehe 02 Septemba 2026 kwa ajili ya kutoa taarifa ya maendeleo ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo. Dkt. Haroun ameeleza Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China imeendelea kutoa fursa za masomo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wananchi wa Zanzibar ili kusaidia wananchi kupata kuongeza taaluma ya kisasa katika fani mbalimbali za elimu wanazosomea. Aidha, Waziri Haroun ameiomba Serikali ya China kuangalia uwezekano wa kuanzisha programu maalumu za mafunzo mafupi kwa viongozi wapya wa Serikali ya Zanzibar, wakiwemo Mawaziri, Naibu mawaziri, Makatibu wakuu na Viongozi wengine wa ngazi za juu. Amesema programu hizo zitawasaidia viongozi wapya kupata uzoefu wa uongozi na utawala, hasa kutokana na baadhi yao kuteuliwa katika nafasi za uongozi bila kuwa na uzoefu mkubwa katika maeneo wanayosimamia. Akizungumza kuhusu uhusiano huo, alisema Serikali ya China imekuwa mashirikiano makubwa wa Tanzania na Zanzibar kwa zaidi ya miaka 60, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha urafiki huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Waziri Haroun, ametoa pongezi kwa Serikali ya China kwa kutoa mashirikiano ya kuwapatia Madaktari bingwa ambao wameisaidia Serikali ya Zanzibar katika kutoa matibabu dhidi ya maradhi mbalimbali yanayowakumba wananchi wa Zanzibar na kuiomba Serikali hiyo kuweza kuwasaidia katika kupambana na maradhi ya kichocho ambayo kwa sasa yamekua yakijitokeza zaidi. Kwa upande wake Balozi mdogo wa Jamuhuri ya watu wa China Zanzibar Konseli. Li Qianghua amesema ushirikiano kati ya China na Zanzibar umeendelea kuzaa matunda katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo watendaji jambo ambalo miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele. Amesema Timu ya 35 ya Madaktari wa China inayotoa huduma Zanzibar inatarajiwa kumaliza muda wake wa mwaka mmoja Septemba 22 mwaka huu, baada ya kutoa huduma mbalimbali za matibabu na kufanya upasuaji kwa wagonjwa. Kwa mujibu wa Balozi Quinghua, madaktari hao pia wamefanya zaidi ya huduma 24 za matibabu nje ya hospitali, hatua iliyowezesha jamii kupata huduma za afya katika maeneo yao. Ameeleza ushirikiano huo wa kitabibu umedumu kwa zaidi ya miongo sita, huku madaktari kutoka China wakifanya kazi kwa karibu na wataalamu wa afya wa Zanzibar na kutoa mafunzo yanayosaidia kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani. “Katika miaka ya hivi karibuni wamefanya baadhi ya upasuaji wa kisasa zaidi, hivyo wagonjwa hawahitaji kutoka nje ya Zanzibar kupata huduma ambazo awali hazikuweza kutolewa hapa,” alisema Balozi. Sambamba na hayo alisema kupitia ushirikiano huo, Zanzibar pia imeanza kunufaika na data na vifaa vinavyosaidia katika uchunguzi wa bahari, usimamizi wa rasilimali na uhifadhi wa mazingira.